CHAMA cha Wanataaluma cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) kimeenda Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kupinga kushikiliwa kwa muda mrefu bila dhamana kwa mhadhiri mwenzao, Melkisedeki Kitunzi Kaijage, anayetuhumiwa na Jeshi la Polisi kuhamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
​Kwa mujibu wa taarifa ya ndani iliyotolewa na Katibu Mkuu wa UDOMASA tarehe 18 Julai, 2026, Kaijage aliripoti Kituo cha Polisi UDOM tarehe 8 Julai akitakiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO).
Baadaye alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma na kisha Kituo Kidogo cha Chang’ombe ambako anaendelea kushikiliwa hadi sasa.
​UDOMASA inaeleza kuwa jitihada zao za kumsemea dhamana ziligonga mwamba baada ya maafisa wa polisi kueleza kuwa kuna “maagizo kutoka juu” ya kumrejesha mahabusu, licha ya kukiri kuwa kosa linalomkabili linadhaminika kisheria:
“UDOMASA inatambua na kusimamia haki za wafanyakazi, na tunapinga na kulaani vikali ukiukwaji wowote wa taratibu za kisheria unaomnyima mfanyakazi uhuru wake. Chini ya sheria za nchi yetu, mtuhumiwa anapaswa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24,” ilieleza taarifa hiyo.
​Baada ya juhudi za dhamana kukwama, UDOMASA kupitia jopo lake la wanasheria ilifungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma tarehe 12 Julai, 2026. Shauri hilo lilisikilizwa kwa mara ya kwanza tarehe 17 Julai na linatarajiwa kuendelea tena Jumanne, 21 Julai 2026, majira ya saa 3:00 asubuhi. Uongozi wa UDOMASA umewataka wanataaluma kuwa watulivu wakati taratibu za kisheria zikiendelea.