CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeeleza kimesikitishwa na wanafunzi 73,129, elimu ya juu wanaoanza mwaka wa kwanza wa masomo 2026/2027 kukosa mikopo huku gharama za masomo zikipanda.Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa Habari, Riziki Shahari Mngwali, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia leo tarehe 11 Oktoba, 2026, amesema kuwa hali hiyo inatokana na upangaji mbaya wa mikopo.
“Kwa mwaka wa masomo 2026/2027, hadi Agosti 31, 2026, waombaji walikuwa 157,309. Hata hivyo, katika awamu ya kwanza iliyotangazwa jana Oktoba 10, wanafunzi 84,180 pekee ndio wamefanikiwa kupata mikopo, huku wanafunzi 73,129 wamekosa mikopo hiyo,”amesema Mngwali.
Mngwali amesema kuwa serikali imeamua kutia mpira kwapani kwa kukwepa wajibu wake wa msingi.
Hata hivyo chama hicho kimeitaka Serikali kuwajibika kwa kutoa elimu ya bure kuanzia ngazi ya msingi mpaka shahada ya kwanza
“ACT tunaitaka Serikali kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora na bure kuanzia elimu ya awali hadi shahada ya kwanza. Serikali ichukue wajibu wa kugharamia elimu ya umma badala ya kuhamishia mzigo kwa wazazi na kuwaingiza wanafunzi katika madeni,”.
Ameongeza kuwa “Vilevile, tunaitaka ifute mfumo wa mikopo kwa ajili ya ada, utafiti na mahitaji ya kimasomo, na badala yake ilipe gharama hizo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa katika vyuo vikuu na vyuo vya kati.Bodi ya mikopo ibaki kutoa mikopo ya kujikimu kwa ajili ya chakula na malazi,”.
Mngwali ameeleza kuwa mbali na wanafunzi kukosa mikopo hiyo bado kuna ongezeko la gharama za elimu
“ACT Wazalendo tumefuatilia taarifa za gharama za kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa mwaka wa masomo 2026/2027 na kubaini ongezeko la gharaai za moja kwa moja zinazolipwa na wanafunzi. Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa katika uchambuzi wetu, gharama hizo zimeongezeka kutoka Sh. 97,400 hadi Sh. 255,400 kwa mwanafunzi, sawa na ongezeko la Sh. 158,000. Gharama mpya zinajumuisha huduma za TEHAMA, maktaba, michezo na mahafali.
Aidha, ada ya kitambulisho imeongezeka kutoka Sh. 5,000 hadi Sh.15,000, huku gharama za mitihani zikiongezeka kutoka Sh.12,000 hadi Sh. 30,000,”.
Ameongeza kuwa “gharama za hosteli pia zimeongezeka. Katika Kampasi ya Mlimani, malipo ya hosteli za ndani yamepanda kutoka Sh.800 hadi Sh. 1,300 kwa siku, huku hosteli za nje Mabibo zikiongezeka kutoka Sh. 500 hadi Sh.1,000 kwa siku. Ongezeko hili limegusa pia Kampasi za DUCE, Mkwawa na UDSM Kagera,”.
“ACT tunaona kuwa ongezeko hili linahitaji maelezo ya wazi kuhusu sababu zake na namna gharama hizo zilivyokokotolewa. Tunaitaka UDSM kuweka wazi msingi wa maamuzi hayo na kupitia upya tozo zinazolalamikiwa.
*Mwisho*