Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, ametangaza msimamo mkali akisema kuwa TLS haitababaishwa wala kutishwa na mashambulizi ya kimkakati yanayofanywa na watawala dhidi ya taasisi hiyo na uongozi wake.Anaripoti mwandishi wetu, Dar es salaam … (endelea).
​Akizungumza na waandishi wa habari na mawakili leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutoka Kituo cha Polisi kusomewa tuhuma zinazomkabili kufuatia wito wa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), Mwabukusi amewataka mawakili na Watanzania wote kusimama imara na kutoyumba katika kulinda utawala wa sheria.
“Huu ni wakati wa kunguruma kwa sauti ambayo haijawahi kusikika kwenye taifa hili, sio wakati wa unyonge. Ni wakati wa kuthibitisha maana halisi ya utawala wa sheria. Tutume ujumbe kwa wote wanaofikiri wanatubabaisha kwamba hatubabaiki. Mimi binafsi sibabaiki, na ninaomba wananchi na mawakili msibabaike,” alisema Mwabukusi.
​Rais huyo wa TLS amesisitiza kuwa mashambulizi anayokumbana nayo hivi sasa ni ya kimkakati yenye lengo la kuisambaratisha taasisi hiyo, lakini akabainisha kuwa Baraza la Uongozi la TLS linakaa kufanya maamuzi mazito yasiyowahi kutokea tangu kuasisiwa kwa chama hicho.
“Hatuwezi kuendelea kawaida tu kama mambo yako sawa wakati sio sawa. Taasisi inashambuliwa na watawala, shambulio hili ni la kimkakati na lazima tulikabili. Tutachukua hatua nzito ambazo hazijawahi kuchukuliwa toka TLS ianzishwe. Mbali na hatua hizo, tunampeleka Jaji Mtulia kwenye Kamati ya Nidhamu kwa sababu hatuwezi kuwa na jaji asiyeheshimu sheria wala maamuzi ya mahakama. Yeyote anayefikiri hii ni ‘free walk in the park’ ajue sisi ni tai kichaa, sio njiwa,” amesisitiza Mwabukusi.