MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, inatarajiwa kutoa hukumu kesho, Ijumaa tarehe 16 Oktoba 2026, katika kesi ya kikatiba Na. 7300 ya mwaka 2026, inayohusu haki ya Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye yupo mahabusu katika Gereza Kuu la Ukonga akikabiliwa na tuhuma za uhaini.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Msingi wa shauri hilo ni malalamiko ya Lissu kunyimwa haki ya faragha ya kuzungumza na mawakili wake kipindi chote kesi yake akiendelea kusikilizwa kwenye mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Tayari mahakama hiyo imehitimisha kusikiliza shauri hilo na Tarehe 6 Novemba 2026 mahakama hiyo inatarajiwa kutoa hukumu katika kesi hiyo.
Kesi hiyo imefunguliwa na mawakili wa Lissu dhidi ya Jeshi la Magereza, ikilenga kutafuta tafsiri ya kikatiba kuhusu mipaka ya mamlaka ya maafisa wa magereza katika usimamizi wa mawasiliano kati ya mawakili na wateja wao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 15 Oktoba 2026, na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa kuanzia saa 3:00 asubuhi na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu nchini, Jaji Amir Mruma, akishirikiana na Jaji Angelo Rumisha na Jaji Evaristo Longopa.
Masuala makuu yanayotarajiwa kuamuliwa ni uhalali wa kikatiba wa maafisa wa magereza kusikiliza au kuingilia mazungumzo ya wakili na mteja wake wakati wa mashauriano ya kisheria, pamoja na haki ya mawakili kutoa ushauri na uwakilishi kwa wateja wao bila kuingiliwa kwa namna inayoweza kuathiri usiri wa mawasiliano hayo.
Shauri hilo linagusa misingi ya haki ya kupata ushauri na uwakilishi wa kisheria pamoja na umuhimu wa kulinda usiri wa mawasiliano kati ya wakili na mteja wake, hususan pale mteja anapokuwa kizuizini.
Chadema imewataka wanachama wake, wafuasi na wananchi kwa ujumla kufika mahakamani kufuatilia mwenendo wa shauri hilo na hukumu itakayotolewa.
Uamuzi huo unatarajiwa kuweka msimamo wa mahakama kuhusu suala lililoibuliwa katika shauri hilo, ingawa maudhui na athari za kisheria za hukumu zitaeleweka rasmi baada ya kutolewa.