.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe, amesema walimu ni nguzo kubwa katika Utumishi wa Umma pamoja na maendeleo ya Taifa.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Amesema ili nchi iendelee inahitaji wasomi watakaobeba jukumu la kuzalisha wasomi wengine watakaobobea katika fani.
Prof. Shemdoe ametoa kauli hiyo l 9 Oktoba 2026 wilayani Bukombe mkoani Geita, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani Wilaya ya Bukombe kwa mwaka 2026.
“Tuna zaidi ya walimu 312,000 katika utumishi wa umma, idadi hiyo ni zaidi ya nusu ya watumishi wote wa umma hivyo walimu ni nguzo kubwa kwenye utumishi na maendeleo ya Taifa,” amesema Prof. Shemdoe.
Ameongeza kuwa licha ya kuwa mwalimu ni mlezi lakini ni kielelezo cha maadili na ujenzi wa uwezo wa kizazi kijacho wakiwepo madaktari, wahandisi, wataalam wa kilimo, watafiti, viongozi katika utumishi wa umma na siasa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu mstaafu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Doto Biteko amesema kuwa mwalimu humpa mtoto maarifa, humfundisha nidhamu na kumpa tumaini anayetoka.
Ameongeza kuwa, kutokana na jukumu hilo kubwa linalotekelezwa na walimu ndio maana ameratibu siku ya walimu Bukombe ili kuheshimu na kutambua mchango wa walimu anayewezesha wanafunzi kutimiza ndoto zao.
Sherehe za Siku ya Mwalimu Duniani huadhimishwa tarehe 5 Oktoba kila mwaka na madhimisho haya yamekuwa yakifanyika Wilayani Bukombe tangu mwaka 2019.
Kwa mwaka huu Kauli Mbiu ya Siku ya Mwalimu Duniani ni “Kusimama na Walimu: Miaka 60 ya kulinda taaluma, kuinua hadhi yake na kuunda mustakabali wetu”.
Mwisho.