RAIS wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amesema utekelezaji wa shughuli za Serikali hauendani na ahadi alizopewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kikao chao cha 27 Agosti 27, 2026, Ikulu ya Chamwino, Dodoma.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Mwabukusi amesema masuala yaliyojadiliwa katika kikao hicho, yakiwemo utawala wa sheria, haki za binadamu, maslahi ya mawakili na mwenendo wa mashauri yaliyoko mahakamani, hayaonekani kutekelezwa kwa namna walivyokubaliana.
Kauli hiyo inaibua maswali kuhusu utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika mazungumzo kati ya uongozi wa TLS na Rais, hasa katika kipindi ambacho masuala ya haki za binadamu na kesi zenye mwelekeo wa kisiasa yanaendelea kujadiliwa nchini.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyochapishwa 12 Oktoba 2026 na DW Kiswahili,Mwabukusi alisema hali anayoishuhudia katika utendaji wa Serikali inatofautiana na maelezo na ahadi alizopokea kutoka kwa Rais.
“Nilichozungumza na Rais na alichoniahidi Rais hakilingani kabisa na ninachoshuhudia Serikali ikifanya. Sidhani kama tunaenda uelekeo mmoja,” alisema Mwabukusi
Mwabukusi aliongeza kuwa angepata nafasi nyingine ya kukutana na Rais, angemweleza moja kwa moja kuhusu kile anachokiona kuwa ni kutotekelezwa kwa makubaliano yaliyofikiwa, hususani katika masuala yanayohusu mawakili, utawala wa sheria na haki za binadamu.
“Rais, kile ulichotuahidi na kile ulichotuambia siyo kinachofanyika kuhusu mawakili, utawala wa sheria, haki za binadamu na masuala yote yaliyoko mahakamani pamoja na suala la Tundu Lissu,” alisema Mwabukusi.