Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi
MTANDAO wa taasisi na vyama vya kitaaluma vya sheria barani Afrika na duniani umeitaka Serikali ya Tanzania kuacha kuingilia na kutumia vyombo vya nidhamu kumkandamiza Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS),Wakili Boniface Mwabukusi.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Taasisi zilizomo kwenye mtandao huo zimeeleza wasiwasi mkubwa juu ya mwenendo wa kinidhamu unaoendeshwa na kamati ya Taifa ya Mawakili (NAC) unaolenga kumfuta kabisa Mwabukusi kwenye orodha ya mawakili.
Shauri hilo (maombi Na.04 ya mwaka 2026) linatokana na kauli halali alizozitoa Mwabukusi Mei 2026 kuitaka Serikali imwachie aliyekuwa Rais wa TLS na kiongozi wa Chadema,Tundu Lissu aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Katika tamko hilo la pamoja,vyama hivyo vya kimataifa vimebainisha kuwa adhabu inayotafutwa ya kumfuta kabisa uanakijiji huyo wa sheria ni kali na inalenga kuweka hofu kwa mawakili wote wanaojitokeza kutetea haki za binadamu.
Vimeibua wasiwasi juu ya ushiriki wa maofisa waandamizi wa serikali akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika kamati hiyo ya nidhamu,hali inayokiuka kanuni za msingi za Umoja wa Mataifa kuhusu wajibu wa mawakili.
Aidha vyama hivyo vimekaribisha uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa tarehe 7 Oktoba 2026 uliosimamisha mwenendo huo wa NAC kusubiri shauri la kikatiba Namba 25918 la mwaka 2026 liliofunguliwa na Mwabukusi mjini Dodoma.
Vimeitaka NAC kuheshimu amri hiyo ya Mahakama Kuu huku vikizitaka mamlaka kufanya mageuzi ya sheria ya mawakili ili kuondoa kabisa udhibiti wa Serikali kwenye vyombo vya nidhamu vya taaluma hiyo.
Mashirika hayo yametoa wito kwa mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa(UN) na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuchukua hatua za dharura na kutoa mawasiliano rasmi kwa Serikali ya Tanzania kuzuia ukiukwaji wowote wa haki za mawakili.
Yamesisitiza kuwa uhuru wa TLS na viongozi wake ndio msingi pekee unaolinda utawala wa sheria na kuzuia matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya raia na wanachama wa taaluma hiyo nchini.
Mwisho.