Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi
BAADHI ya wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wamepinga hatua ya Kamati ya Maadili ya chama hicho, kutaka kusikiliza shauri dhidi ya mwenyekiti wao, Boniface Mwabukusi, wakati tayari kuna zuio la mahakama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, leo Jumapili, tarehe 11 Oktoba 2026, Jebra Kambole, amesema kuwa Kamati hiyo, imeamua kuendelea na shauri hilo, kinyume na sheria na katiba ya nchi.
Amesema, lengo la shauri hilo, ni kutaka kumvua uwakili Mwabukusi kwa lengo la kumnyamazisha yeye na mawakili wengine wenye mrengo wa kupigania haki na utawala wa sheria nchini.
“Mwabukusi anataka kuadhibiwa kunatokana na msimamo wake wa kupigania haki na utawala wa sheria nchini. Mwabukusi anataka kuadhibiwa kwa sababu ya kutetea wanyonge na msimamo wake wa kutetea taaluma,” ameeleza Jebra.
Amesema tayari Mahakama Kuu, Masjala ya Dodoma, imetoa amri ya kuzuia kuendelea kwa shauri hilo, lakini taarifa zinasema, Kamati ya Maadili, imeamua kupuuza amri hiyo ya mahakama.
Akizungumzia chanzo cha shauri hilo, Jebra anasema, chanzo cha mashtaka dhidi ya Mwabukusi ni yeye kutoa hamasa ya kupinga mashtaka ya uhaini dhidi ya Tundu Lissu, wakili wa kujitegemea na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyoyatoa kwenye mkutano mkuu wa mawakili uliofanyika mapema mwaka huu.
Anasema, Mwabukusi alitoa tamko kuhusu mwenendo wa kesi ya Lissu na kwamba baada ya hapo wanachama waliunga mkono na kiongozi huyo, alitekeleza wajibu wake.
“Baada ya hapo, ndipo visa vilianza. Baadhi ya mawakili wakafungua mashitaka kwenye Kamati ya Maadili,” amesimulia Jebra na kuongeza, “Msimamo thabiti usioyumbishwa wa Mwabukusi ndio chimbuko la shauri hilo.”
Amesema, “Kama Kiongozi Mkuu wa TLS aliyechaguliwa kidemokrasia na wanachama, Rais Mwabukusi anawajibu wa kisheria na kijamii kusema pale misingi ya nchi inapoyumba.”
Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuwanyamazisha mawakili wote wenye kukemea uovu. Amesema kuwa wao wamechua hatua ya kufungua kesi kwa lengo la kuhakikisha kuwa uhuru wa mawakili unalindwa na kwamba kesi dhidi yake ipo kinyumbe cha Katiba.
Naye Paul Kisabo, mwanachama mwingine wa TLS amesema, kesi iliyoifanya Mahakama kutoa amri dhidi Kamati ya Maadili ya chama hicho (National Advocates Committee), imesajiliwa mahakamani na kupewa Na. 25918/2026 na kwamba wao wanaamini kuwa “shambulizi dhidi ya wakili mmoja ni shambulizi dhidi ya mawakili wote.”
Kesi hiyo ya kikatiba, inayopinga ukiukwaji wa haki za kikatiba za Mwabukusi, unaodaiwa kufanywa na kamati hiyo ilisikilizwa na Mahakama Kuu, Alhamisi iliyopita, tarehe 8 Oktoba mwaka huu.
Baada ya mawasilisho ya Wakili wa mwombaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Maadili, pamoja na mengine, Mahakama ilitoa amri ya kuruhusu taarifa ya shauri kutolewa kwa mjibu maombi wa tatu kupitia matangazo katika magazeti ya Mwananchi na Daily News na kuzuia kuendelea kwa mwenendo wa shauri mbele ya Kamati ya Maadili.
Mahakama imepanga kusikiliza shauri hilo, tarehe 16 Oktoba 2026, saa 5:00 asubuhi kwa ajili ya kupokea maelekezo na amri nyingine zitakazohitajika.
Katika hatua nyingine, mmoja wa mawakili ameliambia MwanaHALISI Online kuwa kesi dhidi ya Mwabukusi, inasukumwa na maelekezo kutoka juu, kutokana na kutofurahishwa na mwenendo wake wa uongozi, kufuatia kugoma kuweka mfukoni. Hakutaja anachoita, “mkono kutoka juu,” ni wapi.