WAZAZI na walezi katika jiji la Mwanza, wametakiwa kuwapa watoto wa kike elimu bora ili kukuza uwezo wao na kutimiza ndoto walizonazo.Anaripoti mwandishi wetu, Mwanza … (endelea).
Wito huo umetolewa jana tarehe 9 Oktoba, 2026 na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji hilo, Gradness Lubemkamu, ambapo amesema elimu ndiyo itakayomsaidia kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye jamii anayoishi.
Amebainisha kuwa elimu sahihi kwa jamii pia itachochea kupungua kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Elimu kuhusu changamoto zinazomkabili mtoto wa kike, imetolewa kwa jamii na Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kwa kushirikiana na mashirika ya Amani Girls na Kivulini ambapo kila mwaka dunia inafanya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa yanayofanyika 11 Oktoba kila mwaka.
Elimu hiyo imetolewa katika Shule ya Sekondari Shamaliwa, Kata ya Igoma jijini Mwanza, ikijikita katika afya ya akili, ukatili wa kijinsia, pamoja na malezi na makuzi bora ya mtoto wa kike.
Kwa upande wake, Magreth Kadwela, kutoka Shirika la Kivulini, amesema kufanikisha ndoto za mtoto wa kike kunahitaji ushirikiano wa wazazi, walimu, taasisi na Serikali katika kumsaidia mtoto kukua na kufikia malengo yake.
Baadhi ya wazazi na wanafunzi walioshiriki elimu hiyo wamesema itasaidia kumlinda mtoto wa kike dhidi ya vitendo visivyofaa, ikiwemo ndoa na mimba za utotoni, ambavyo vinaweza kuathiri masomo na kutimiza ndoto zake.
Mwisho.