SPIKA wa Bunge la Australia, Milton Dick, amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), baada ya kupata asilimia 56 ya kura na kuwashinda wagombea wengine wawili katika uchaguzi uliofanyika leo, 9 Oktoba 2026.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Matokeo ya uchaguzi huo yametangazwa na Rais wa IPU anayemaliza muda wake, Dk. Tulia Ackson, ambaye amemkabidhi Dick nafasi hiyo baada ya kuhudumu kama rais wa 31 wa taasisi hiyo ya kimataifa inayounganisha mabunge kutoka nchi mbalimbali duniani.
Katika matokeo hayo, Profesa Zahara Gafarova ameshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 38 ya kura, huku Rojo Edwards Silva akipata asilimia sita.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, Dick amesema atajikita katika kuimarisha demokrasia, amani na ushirikiano wa kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kujenga taasisi inayosikiliza na kuheshimu maoni ya mataifa yote, bila kujali ukubwa wake au uwezo wake wa kiuchumi.
Amesema ataanza kutekeleza majukumu yake mara moja, akitumia mpango wa utekelezaji wa siku 100 za kwanza kuweka mwelekeo wa uongozi wake.
Dick ameeleza kuwa ushindi wake umetokana na imani waliyoonyesha wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za dunia, huku akiwashukuru pia wale waliowaunga mkono wagombea wengine katika uchaguzi huo.
“Leo hakuna washindi wala walioshindwa. Leo IPU imezungumza kwa sauti moja. Hii ndiyo demokrasia,” amesema Dick.
Uchaguzi huo unafungua ukurasa mpya wa uongozi wa IPU, huku Dick akitarajiwa kuendeleza juhudi za taasisi hiyo katika kuimarisha mazungumzo baina ya mabunge, demokrasia na ushirikiano wa kimataifa.
Dk. Tulia Ackson, ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, alichaguliwa kuwa Rais wa 31 wa IPU 27 Oktoba 2023, katika Mkutano Mkuu wa 147 uliofanyika Luanda, Angola.
Uchaguzi huo ulimfanya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika na wa tatu duniani kushika nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa IPU mwaka 1889.
IPU ni taasisi ya kimataifa inayowaunganisha wabunge kutoka mabunge ya nchi mbalimbali, ikiwa na jukumu la kukuza mazungumzo ya kibunge, demokrasia, amani, ushirikiano wa kimataifa na ushiriki wa wananchi katika utawala.
Uongozi wa Dick unaanza baada ya kipindi cha Dk. Tulia Ackson, ambaye kupitia nafasi hiyo aliiwakilisha Tanzania katika jukwaa muhimu la ushirikiano wa mabunge duniani.