KIKUNDI cha Mawaziri cha Jumuiya ya Madola (CMAG) kimeiagiza Serikali ya Tanzania kushughulikia suala la kuzuiliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kupitia njia za kisiasa na kisheria ndani ya siku 30, pamoja na kuwaachia huru watu wengine wanaoshikiliwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni matumizi ya haki zao kwa njia ya amani.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Maelekezo hayo yameelezwa katika tamko lililotolewa baada ya mkutano wa dharura wa CMAG uliofanyika 10 Julai 2026.
Tamko hilo pia linaitaka Tanzania kuanzisha jukwaa la mashauriano linaloshirikisha vyama vyote vya siasa ndani ya siku 90 kwa ajili ya kujadili mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ushindani wa kisiasa, masuala ya mahabusu pamoja na uwajibikaji.
Aidha, CMAG imeitaka Serikali kurejesha uhuru kamili wa matumizi ya mitandao ya kijamii ndani ya siku 60 na kuondoa vikwazo vinavyohusu uhuru wa kukusanyika, kujieleza, shughuli za asasi za kiraia na vyombo vya habari.
Kikundi hicho kimesema kitaendelea kuiweka Tanzania katika ajenda yake rasmi, kikieleza kuwa licha ya hatua chache zilizopigwa tangu mkutano wake wa 5 Desemba 2025, bado kuna maeneo muhimu ambayo hayajatekelezwa kikamilifu.
CMAG pia imesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa kati ya vyama, kuwawajibisha wahusika wa matukio ya vurugu na kutoa fidia kwa waathirika pale inapostahili.
Kwa upande wake, Serikali ya Tanzania imeendelea kusisitiza kuwa haiwezi kuingilia mwenendo wa shauri la Tundu Lissu kwa kuwa suala hilo liko mahakamani.
Viongozi wa Serikali wameeleza mara kadhaa kuwa Tanzania ni nchi huru yenye mamlaka kamili ya kuendesha masuala yake ya ndani kwa mujibu wa Katiba na sheria zake bila kushinikizwa na mataifa au taasisi za nje.
Tamko hilo limefuatia kupokelewa kwa ripoti ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuhusu ziara ya Mjumbe Maalum wa Jumuiya hiyo, Dk. Lazarus McCarthy Chakwera, aliyefanya ziara nchini Tanzania mwezi Aprili 2026 na kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi wa Serikali, vyama vya siasa na wadau mbalimbali ili kutathmini maendeleo ya hali ya kisiasa na utawala nchini.