MAHAKAMA Kuu, Masjala Kuu ya Dodoma, imegiza Kamati ya Taifa ya Maadili ya Mawakili kusubiri uamuzi wa shauri la kikatiba linalopinga mchakato wa kumvua uwakili Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Amri hiyo imetolewa leo, tarehe 19 Oktoba, 2026 na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi, Jaji Amir Mruma imesitisha usikilizwaji wa shauri la kinidhamu linalomkabili Mwabukusi mbele ya kamati hiyo mpaka pale shauri hilo litakapotolewa uamuzi.
Baada ya uamuzi huo, jopo la mawakili wanaomtetea Mwabukusi, linaloongozwa na Wakili Mwandamizi Mpale Mpoki, limeeleza matumaini yake kuwa Kamati ya maadili ya mawakili itazingatia maelekezo ya mahakama na kuheshimu utawala wa sheria.
Shauri la kinidhamu dhidi ya Mwabukusi lilifunguliwa na Wakili Chacha Nashon, anayedai kuwa baadhi ya kauli zilizotolewa na kiongozi huyo kuhusu mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, zilikiuka kanuni za mawakili.
Kupitia shauri hilo, Nashon anataka Mwabukusi avuliwe uwakili kutokana na madai hayo,hata hivyo, madai hayo yanapaswa kutofautishwa na uamuzi wa mwisho wa chombo chenye mamlaka ya kuyatolea maamuzi.
Mgogoro huo umechukua mwelekeo mwingine wa kisheria kupitia shauri la kikatiba lililofunguliwa mahakama kuu, ambalo pamoja na mambo mengine linapinga uhalali wa mchakato wa kumvua Mwabukusi uwakili.
Iwapo Kamati hiyo itamkuta Mwabukusi na hatia na kuamua kumvua uwakili, hatua hiyo inaweza kuathiri sifa zake za kuendelea kuwa Rais wa TLS, kwa kuwa nafasi hiyo inahusishwa na sifa za kitaaluma za kuwa wakili.
*mwisho*