HATUA ya Boniface Mwabukusi, Rais waChama cha Mawakili Tanganyika (TLS), kutaka kuvuliwa uwakili wake na Kamati ya Maadili ya Mawakili imetajwa inalenga kuzima sauti za kitaaluma zinazoikosoa Serikali.Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Sababu hiyo imetolewa na Isihaka Mchinjita, Makamo wa Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, (Bara) ambaye amesema kuwa kesi ya Mwabukusi inaakisi namna Tanzania inavyorejea nyuma kidemokrasia.
“Badala ya nchi kuonekana inasonga mbele tunarudi nyuma kwa kuwakabili wale wanaopaza sauti ya kukemea yasiyofaa,”amesema Mchinjita.
Amesema kuwa TLS, ilipaswa itazamwe kwa jicho la kuwa ni wasaidizi wa muhimili wa kisheria si uadui.
“Badala ya TLS kuwa msaidizi wa kuisaidia serikali kutazama masuala kisheria, kuisaidia mahakama kama muhimili ili kuona kwamba haki inapatikana na kuwa na nchi ambayo watu wanajivunia, leo tunaiweka TLS kwenye wakati mgumu,” amesema Mchinjita.
Amesema kuwa kumekuwa na rejea ya kusulubiwa kwa viongozi wa TLS wenye msimamo tofauti na watawala.
“Itakumbukwa kwamba hili ni tukio la tatu kuwakuta viongozi wa TLS, tunakumbuka tukio lililomkuta Fatma Karume, akiwa Rais wa TLS, Tundu Lissu, akiwa Rais na sasa Mwabukusi akiwa Rais TLS kwa hiyo maana yake kwamba TLS inafanywa itumike kama chombo kwa maslahi ya Serikali kuliko ya sheria na umma. Hii ni hatua mbaya sana.
“Katika nchi ambayo inaheshimu utawala wa sheria vyombo hivi ambavyo msingi wake ni sheria vinapaswa kuheshimiwa na maoni yake kusikilizwa na kufanyiwa kazi,” amesema Mchinjita.
Mchinjita amesema kuwa Mwabukusi ameingia kwenye changamoto hiyo akiwa anatekeleza wajibu wake wa kisheria.
Mwisho.
