ALIYEKUWA Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Musa Juma Assad, amesema anaamini kuwa kuondolewa kwake madarakani mwaka 2019 kulifanyika kinyume cha Katiba, huku akidai kuwa hadi sasa hajawahi kupewa majibu ya hoja alizowasilisha akihoji uhalali wa uamuzi huo.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Profesa Assad alisema baada ya kutenguliwa katika nafasi hiyo aliandika barua rasmi akiomba ufafanuzi wa sababu za hatua iliyochukuliwa dhidi yake, lakini hakupata majibu licha ya kufanya ufuatiliaji mara kadhaa.
“Kitendo cha kutenguliwa kwangu kilikuwa kinyume cha Katiba. Ilivyotokea niliandika barua ya kuhoji kwanini limetokea jambo hilo, niliifuatilia hiyo barua lakini haijakibiwa hadi leo,” alisema Prof.Assad
Aliongeza kuwa akiwa mtumishi wa umma mwenye uzoefu wa muda mrefu alitambua kuwa kuhoji baadhi ya maamuzi ya mamlaka kunaweza kuwa na athari zake, lakini aliona ni wajibu wake kutafuta ufafanuzi wa kisheria na kiutawala.
“Maneno yana gharama, hata wakati naandika zile barua zangu kuhoji kuhusu kuondolewa kwangu nilijua tu kuna siku zitanigharimu,” alisema.
Profesa Assad aliteuliwa kuwa CAG mwaka 2014 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, na kuanza rasmi kuhudumu Januari 2015.
Katika kipindi chake cha uongozi, aliibua mijadala mbalimbali kupitia ripoti za ukaguzi zilizohusu matumizi ya fedha za umma, uwajibikaji wa taasisi za serikali na usimamizi wa rasilimali za taifa.
Mwaka 2019, Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli, alimteua Charles Kichere kuwa CAG mpya, hatua iliyotafsiriwa kama kumalizika kwa kipindi cha Profesa Assad katika ofisi hiyo.
Profesa Assad aliondolewa rasmi 3 Novemba 2019, kabla ya kufikisha umri wa kustaafu wa miaka 65 uliowekwa kwa mujibu wa sheria za ofisi hiyo.
Kuondolewa kwake kulizua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi kuhusu uhuru wa taasisi za ukaguzi wa fedha za umma na ulinzi wa viongozi wa taasisi za kikatiba. Baadaye, Mahakama Kuu iliamua kuwa hatua ya kuondolewa kwake ilikuwa kinyume cha Katiba, na uamuzi huo ukaweka msingi muhimu katika tafsiri ya mamlaka ya uteuzi na uondoaji wa viongozi wa taasisi za kikatiba nchini.