POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam imemtia mbaroni Juma Ramadan (21), maarufu Juli, mkazi wa Ubungo, kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Ramadan Jafar (47), maarufu Muna, ambaye awali aliripotiwa kupotea.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema kuwa 16 Juni 2026, Kituo cha Polisi Kimara Gogoni kilipokea taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa Ramadan Jafar kuhusu kutoweka kwake.
Muliro amesema uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi ulibaini kuwa mtu aliyeripotiwa kupotea alikuwa ameuawa na mwili wake kufukiwa ndani ya moja ya vyumba vya nyumba yake iliyopo Mbezi Luguruni Kwembe, Wilaya ya Ubungo.
Kwa mujibu wa polisi, baada ya kudaiwa kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa alichimba shimo ndani ya chumba ambacho marehemu alikuwa akikitumia na kuufukia mwili wake ili kuficha uhalifu huo.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo huku mtuhumiwa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.