MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Kawaida, amesema aliyekuwa Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi, alikaidi maelekezo ya chama ya kufika katika vikao vya maadili, hatua iliyosababisha Kamati Kuu ya CCM kuamua kumfukuza uanachama.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kawaida amesema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CCM), kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uongozi (NEC), ilitoa maelekezo ya Nchimbi kuitwa katika vikao vya maadili, lakini hakutekeleza maelekezo hayo.
Amesema kutofika kwake katika vikao hivyo kulichukuliwa kama kutokuheshimu na kutofuata maelekezo ya chama, jambo ambalo hatimaye lilisababisha Kamati Kuu kuchukua hatua dhidi yake.
“Yeye kwa sababu ya kiburi, kwa sababu ya kutokuona umuhimu na kudharau maelekezo ya chama hakufika, ndipo Kamati Kuu ikaazimia kumfukuza chama,” amesema Kawaida.
Kawaida ameyasema hayo leo 29 Agosti 2026, mkoani Dodoma, muda mfupi baada ya kushuhudia kuapishwa kwa Makamu mpya wa Rais, Deogratius Ndejembi.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa UVCCM amesema suala hilo linapaswa kuwa funzo kwa vijana, akisisitiza umuhimu wa kuwa na heshima, nidhamu na uaminifu, hasa pale mtu anapopewa dhamana ndani ya chama.
Amesema pia ni muhimu kwa wanachama kuheshimu taratibu na maelekezo ya chama wanapopewa majukumu au kuaminiwa kushika nafasi mbalimbali.