MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Heche amempongeza Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba kwa kile alichokiita “kusimama na nchi” na kuwa sauti ya Watanzania katika kipindi hiki.Anaripoti Zakia Nnanga, Dar es Salaam … (endelea).
Heche amesema Warioba, kutokana na umri wake na historia yake, hana haja ya kutafuta nafasi za kisiasa kama urais, ubunge au udiwani, bali anachokihitaji ni kuona Tanzania ikiendelea kwenda katika mwelekeo mzuri.
Heche ameyasema hayo leo 29 Agosti 2026, wakati akizungumza na wanahabari katika Kikao Maalumu cha Kamati Kuu ya Chadema kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
“Yule mzee hahitaji kuwa Mbunge, hahitaji kuwa Diwani, hahitaji kuwa Rais, lakini anaposimama katikati ya wazee wengine ambao wamekata kauli, nchi inakwenda shimoni wanaona, anakuwa sauti ya Watanzania. Tunahitaji kumpongeza na kumpigia makofi kweli,” amesema Heche.
Katika hatua nyingine, Heche amemkosoa Mzee Joseph Butiku kufuatia kauli yake ya hivi karibuni kwamba Chadema inapokea fedha na misaada kutoka nje, hususan Marekani.
Heche amesema Butiku, ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo Katibu Mkuu, anafahamu taratibu zinazohusu fedha au misaada kutoka nje kuingia nchini.
Amesema alitarajia kuwa iwapo Butiku anatoa madai hayo, angewasilisha ushahidi wa kuthibitisha kauli yake.
“Amesema mambo mawili ambayo nitayazungumza kwa kifupi, ambayo kiukweli yanauma sana. Mzee Butiku amesema kwamba Chama chetu kinapokea fedha na misaada kutoka Marekani,” amesema Heche.
Heche pia amejibu kauli ya Butiku kuhusu Chadema kushinikiza Rais kumuachilia huru Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, akisema suala hilo si la Chadema pekee bali limekuwa likizungumziwa na watu mbalimbali duniani.
“Halafu anasema kwamba Chadema wanamshinikiza Rais amuachilie Lissu. Ndiyo, kwa sababu hii ni kesi yake huyo Rais, ni kesi ya uongo. Na ndiyo maana dunia, siyo Chadema tu, inashinikiza kutaka Lissu aachiliwe.
Ni dunia nzima inasema Lissu aachiliwe,” amesema Heche.
Kauli hizo zimetolewa wakati Chadema ikiendelea na vikao vyake vya ndani, huku viongozi wa chama hicho wakisisitiza umuhimu wa uhuru wa kisiasa na masuala wanayoona yanaathiri mustakabali wa demokrasia nchini.