SHAURI la uhaini namba 19605/2025, linalomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, lnaendelea leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Shauri hilo linaendelea katika hatua ya ushahidi wa utetezi, huku shahidi wa nne wa upande wa utetezi, Brenda Jonas Rupia, akiendelea kujibu maswali ya dodoso (cross-examination) kutoka kwa mawakili wa Serikali.
Rupia, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, jana alikabiliwa na maswali kuhusu nafasi yake ndani ya chama hicho, ikiwemo kama aliisomea taaluma inayohusiana na nafasi hiyo.
Akijibu, Rupia alieleza kuwa hakusomea nafasi hiyo, huku akifafanua kuwa shughuli za mawasiliano ndani ya Chadema hazifanywi na yeye pekee, bali zinatekelezwa na timu inayohusika na eneo hilo.
Katika hatua nyingine ya mahojiano hayo, Rupia aliulizwa kuhusu madai kwamba Lissu aliwahi kutoa kauli za kuitishia Serikali na kupanga kuvuruga uchaguzi wa mwaka 2025, zikiwemo kauli kama “tutauvuruga uchaguzi” na “tutakinukisha.”
Rupia alikana madai hayo, akieleza mahakamani kuwa si sahihi.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, linalodaiwa kuwa chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023.
Kesi hiyo inaendelea leo huku upande wa utetezi ukiendelea na ushahidi wake kupitia shahidi huyo.