RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Mwinyi, ametoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar na viongozi wa vyama vya siasa kuunga mkono mchakato wa maridhiano ya kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, akisisitiza kuwa utasimamiwa kwa kuzingatia masilahi mapana ya Zanzibar.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Mwinyi alitoa wito huo leo 9 Julai 2026, mjini Unguja wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini wa tamko la pamoja la maridhiano kati ya vyama hivyo, mazungumzo ambayo yalianza 9 Novemba 2025.
Alisema kutiwa saini kwa tamko hilo ni hatua muhimu katika kufungua njia ya utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kwa mujibu wa vifungu vya 9(3) na 39.
“Natoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa na wananchi wote wa Zanzibar kuunga mkono dhamira hii njema ya kuleta maelewano na maridhiano, ili kuchochea mshikamano, amani na mustakabali mwema wa nchi yetu,” alisema Mwinyi.
Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa viongozi watausimamia mchakato huo kwa dhamira ya dhati, wakitanguliza masilahi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.
Maridhiano hayo yanatarajiwa kuimarisha mazingira ya kisiasa nchini Zanzibar na kuweka msingi wa ushirikiano miongoni mwa vyama vya siasa katika kuendeleza amani, utulivu na maendeleo.