WAWAKILISHI wa Asasi za Kiraia zinazofanya kazi katika sekta ya haki za binadamu wamekutana kujadili na kubadilishana taarifa kuhusu masuala muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele katika Mapitio ya Nne ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR), yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Mapitio hayo yanalenga kutathmini hatua zilizochukuliwa na nchi katika kuimarisha ulinzi, ukuzaji na utekelezaji wa haki za binadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo uliofanyika 9 Julai 2026, Mratibu wa Kitaifa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumo amesema mchakato wa UPR unatoa fursa sawa kwa nchi zote kutathminiwa na kupokea mapendekezo ya kuboresha hali ya haki za binadamu.
Amesema nchi hushiriki kwa hiari katika mchakato huo kwa kukubali mapendekezo ambayo ziko tayari kuyatekeleza, lakini amebainisha kuwa takribani nusu ya mapendekezo yaliyokubaliwa katika mzunguko uliopita hayakutekelezwa ipasavyo.
Olengurumo ameongeza kuwa zaidi ya asasi za kiraia 300 zimeshiriki katika maandalizi ya mapitio ya mwaka huu kwa kuandaa na kuwasilisha ripoti yenye mapendekezo mbalimbali, ambayo tayari imefikishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kuzingatiwa katika mchakato wa mapitio.
Amesema ushiriki wa asasi za kiraia ni muhimu katika kuhakikisha tathmini inayofanyika inaakisi hali halisi ya utekelezaji wa haki za binadamu nchini na kuchangia maboresho ya sera na mifumo ya kulinda haki za wananchi.