WAZIRI Kivuli wa Elimu wa ACT Wazalendo, Riziki Shahari, amesema Bajeti ya Serikali Kuu ya mwaka 2026/27 imeshindwa kushughulikia changamoto za ugharamiaji wa elimu ambazo zinaendelea kuwa mzigo kwa wazazi na wanafunzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akichambua bajeti hiyo leo Juni 23, 2026, Shahari alisema licha ya sera ya elimu bila ada kutekelezwa kwa miaka 10, wazazi bado wanachangia gharama mbalimbali zikiwemo chakula, mitihani, masomo ya ziada na ujenzi wa miundombinu ya shule.
Alisema tafiti za Policy Forum na Twaweza zinaonesha mzazi hutumia kati ya Sh120,000 na Sh250,000 kwa mwaka kwa mtoto wa shule ya msingi vijijini, huku gharama hizo zikifikia zaidi ya Sh450,000 mijini.
Kwa upande wa elimu ya juu, Shahari alisema wanafunzi wengi bado wanakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na kukosa au kupata mikopo isiyotosheleza kutoka HESLB. Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha wastani wa wanafunzi 2,990 huacha vyuo kila mwaka kutokana na changamoto za ugharamiaji wa masomo.
ACT Wazalendo imesema bajeti hiyo haijaweka mikakati ya kupunguza gharama hizo na hivyo kuendelea kuhatarisha usawa katika upatikanaji wa elimu.