Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu
KIONGOZI wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amesema mamilioni ya Watanzania wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa gharama za matibabu kutokana na udhaifu wa mfumo wa afya na kusuasua kwa utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akichangia Uchambuzi wa Bajeti ya Serikali 2026/27 leo katika Makao Makuu ya ACT Wazalendo, Semu amesema zaidi ya asilimia 88 ya Watanzania hawapo kwenye mfumo wa bima ya afya, huku utekelezaji wa mpango huo ukishindwa kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
“Wananchi wanaendelea kukosa huduma bora za afya, dawa, vifaa tiba na wataalamu wa afya, wakati Serikali ikiendelea kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki kwa kiwango kilichoahidiwa,” amesema Semu.
ACT Wazalendo inasisitiza kuwa suluhisho la kudumu ni kujenga mfumo imara wa hifadhi ya jamii na kuwekeza zaidi katika huduma za afya ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bora bila kujali uwezo wake wa kifedha.