Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesisitiza umuhimu wa kuwapo maridhiano ya kitaifa, ili kulikwamua taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
“…baada ya kuumizana au kabla ya kuumizana kuzungumza kufikia hatima njema ya taifa letu ni jambo lisiloepukika. Ni lazima kuwepo na mazungumzo ya awali yatakayojumuisha wadau halisi na wenye uhalali wa kijamii na kisiasa (na siyo yale makundi ya kitapeli ambayo tayari yanajulikana kwa vitendo vyake vilivyochangia Taifa kufikia hapa kwa kisingizio cha amani na utulivu),” anaeleza Mwabukusi katika taarifa yake kwa umma, aliyoitoa leo Jumamosi, tarehe 20 Juni 2025.
Mwabukusi anayataja makundi hayo, kuwa ni pamoja na vyama vya upinzani vilivyonyimwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi (Chadema); mgombea wa urais aliyezuiwa na kunyimwa haki yake ya kusikilizwa kwa wakati na Mahakama, Luhaga Mpina (ACT) na taasisi za kitaaluma.
Wengine, ni asasi za kiraia na kijamii, mwakilishi wa waathirika wa mateso, mauaji na upotevu wa kulazimishwa, pamoja na jamii za asili za kienyeji zilizoathiriwa vibaya na miradi inayodaiwa kuwa ya maendeleo na uwekezaji, kama vile Wamasai wa Ngorongoro.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, ili kufanikisha maridhiano hayo, ni vema bodi ya ushauri, ambayo itakuwa na mkusanyiko wa wataalamu wa kimataifa, ambao siyo tu watashauri bali watasimamia na kuhusika katika uratibu wa mazungumzo mpaka kufikiwa kwa maridhiano ya Kitaifa.
Anasema, bodi hiyo, itasimamia na kushauri kuhusu mabadiliko ya kisheria na kikatiba pamoja na mabadiliko ya vyombo vya usimamizi wa utawala bora – Bunge na Mahakama – ili kuviondoa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka kwenye kwapa la Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa vyombo vya kitaifa visivyo jifungamanisha na siasa.
Aidha, bodi hiyo, itasimamia na kushauri kuhusu utaratibu wa mpito na kuundwa upya taasisi za kidemokrasia kama Tume Huru ya Uchaguzi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Watashauri, kuratibu uchunguzi kuhusu uwajibikaji wa kitaasisi na kibinafsi kwa madhila ya kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa 29 Oktoba mwaka jana, ikiwemo vitendo vya utekaji na upotezwaji wa wakosoaji wa Serikali,” amefafanua.
Rais wa TLS anasema, “kimsingi lazima tutoke kwenye mkwamo huu, lakini utokaji wetu lazima uongozwe na ukweli, haki na uwajibikaji.”
Anaongeza, “Ili kufikia maridhiano ya kweli na endelevu, ni lazima kuwepo kwa misingi imara ya ukweli, haki na uwajibikaji.
“Ni lazima upande wa serikali ambao ndio wasababishaji wa yaliyotokea, kuonesha kuwajibika ikiwemo kufuta kesi na mashauri yote yenye mtizamo wa kisiasa, ikiwemo kuachiliwa huru mara moja kwa Wakili Tundu Lissu na kulipwa madai yake yote aliyodhulumiwa na Bunge, stahiki zake za matibabu pamoja na fidia kwa uonevu aliofanyiwa.”
Mwabukusi anashauri katika nyakati hizi, viongozi wenye dhamana, wajiepushe na siasa au propaganda za kimazoea, kwa kuwa duniani kuna mabadiliko sana ya kiteknolojia, jambo linalorahisisha upataji taarifa sahihi kwa wakati.
“Vijana wamekwisha uona moshi. Hamuwezi kuficha moto, busara ni kuzitambua nyakati la sivyo hakuna atakayebaki salama katika jamii ambayo lundo kubwa la vijana limepoteza matumaini,” anafafanua.
Anasema, “Mazungumzo haya ya awali yatawezesha kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo, ajenda na kanuni za mazungumzo makuu, pamoja na kubainisha kwa uwazi umuhimu wa kuyaendesha mazungumzo hayo chini ya usimamizi wa chombo huru cha nje (msimamizi wa tatu) chenye uadilifu, uzoefu na kuaminika.
“Tumekwisha ya vulia maji nguo kwa matendo na Kauli zetu za kutowajibika kwa Kujua au kutokujua hivyo hatuna njia nyingine isipokuwa kuyaoga.”
Akizungumzia umuhimu wa kuimarisha haki ya kujieleza, Mwabukusi anasema, “Haki ya kujieleza na haki ya kuandamana, zinatambuliwa kikatiba na kisheria nchini. Haki hizi zinatambuliwa pia na katika vyombo vya kikanda na kimataifa.
“Nchini Tanzania, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inalinda haki ya uhuru wa maoni na kujieleza kupitia Ibara ya 18, ambayo inahakikisha uhuru wa kutoa mawazo, kupokea na kusambaza taarifa bila kuingiliwa.”
Nayo haki ya kukusanyika na kuandamana kwa amani, inalindwa chini ya Ibara ya 20 ya Katiba, ingawa utekelezaji wake unasimamiwa na sheria ya Vyama vya Siasa na sheria ya Polisi, ambazo huweka masharti ya kibali na usalama wa umma.
“Katika ngazi ya kikanda na kimataifa, haki hizi zimeainishwa wazi. Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and Peoples’ Rights), kupitia Ibara ya 9 unatambua uhuru wa kujieleza, na Ibara ya 11 inalinda haki ya kukusanyika kwa amani.
“Kimataifa, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) kupitia Ibara ya 19 unahakikisha uhuru wa kujieleza, wakati Ibara ya 21 inalinda haki ya kukusanyika kwa amani,” anafafanua.
Hivyo basi, Mwabukusi anasema, “kwa ujumla, haki hizi ni za msingi katika mfumo wa kisheria wa kitaifa, kikanda na kimataifa, ingawa zinaweza kuwekwa mipaka ya kisheria kwa maslahi ya usalama, utulivu wa umma na maadili ya jamii.
“Hii tabia ya kujinaisha maandamano kwa kauli za Jumla Jumla, mikutano ya kisiasa, midahalo mavyuoni na kwenye taasisi za kitaaluma haisaidii ku accommodate diversity zaidi ina dumaza Tifa letu na Kulifanya kuwa nchi inayoongozwa kijeshi na Kipolisi.
“Ni muhimu kuona njia bora pale vyombo vya Ulinzi vinapotaka kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha kila mmoja anaitumia haki yake bila kuvunja sheria.”
Mengine aliyoeleza, ni kama ifuatavyo:
HAKI REJESHI NA HAKI ADHABU
Kulingana na yale yaliyojitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi hususan utekaji na upotezwaji wa watu na mauaji ya raia inahitajika matumizi ya mbinu zote mbili za haki yaani haki rejeshi (restorative justice) na haki adhabu (retributive justice), ili kushughulikia kikamilifu madhila yaliyotokea.
Madhila hayo yahusishe matukio yote ya kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi, pamoja na kuchunguza kwa kina ushiriki wa kila mmoja iwe ni mtu binafsi au taasisi katika kuwezesha mauaji ya halaiki, iwe kwa kufanya au kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Ni muhimu pia kuundwa kwa taasisi madhubuti, inayojumuisha watu waadilifu, wanaoaminika na wenye mapenzi ya dhati kwa haki, pamoja na uwakilishi mpana wa makundi yote muhimu ya jamii Ikiwemo wahanga wa matendo haya.
Taasisi hiyo inapaswa kuwa na majukumu ya mpito yatakayoliongoza Taifa kutoka katika mkwamo wa sasa.
UADILIFU NA AINA YA WAJUMBE:
Katika mbinu za ndani, ni lazima kuepuka utegemezi pekee kwa watu waliokosa uzalendo au waliogubikwa na hofu au upendeleo, na wale wanaoendelea kunufaika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na mfumo uliopo.
Badala yake, mchakato huu unapaswa kuongozwa na watu wazalendo, waadilifu, wasio na upendeleo na wenye mapenzi ya dhati kwa Taifa.
Aidha, katika mazungumzo haya, haki za Watanganyika na haki za Wazanzibari lazima zizingatiwe kwa usawa na kwa uadilifu.
Ni muhimu pia kwamba utekaji, upotezwaji na mauaji makubwa yaliyofanyika dhidi ya Watanganyika yachunguzwe kwa kina na kwa ukamilifu, sambamba na kuwajibishwa kwa wahusika.
Vilevile, vitendo vya wizi wa mali za umma, uzembe na ufujaji wa mali asili za Tanganyika vinapaswa kuchunguzwa kwa umakini, hususan pale ambapo mikataba iliingiwa kinyume cha sheria au bila uwazi, bila kujadiliwa ipasavyo bungeni, na bila kuwapa wananchi fursa ya kuipitia na kuihakiki wanufaika wake na madhara yanayotokana na usiri katika ikataba hii kwa raia, utawala bora na uwajibikaji .