WANACHAMA wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Kata ya Lyabukande mkoani Shinyanga wamehukumiwa kifungo cha miezi minne gerezani au kulipa faini ya Sh300,000 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia katika kesi iliyosikilizwa katika Mahakama ya Mwanzo Kizumbi.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, hukumu hiyo ilitolewa 19 Juni 2026 dhidi ya Masele Bahati Lubongeja, Raphael Henri Masangwa, John Charles Mashenene na Zephania Lugwisha Maduhu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa wanachama hao walitiwa hatiani kwa kosa la kufanya fujo wakati wa mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.
Akizungumzia hukumu hiyo, Mnyawami alisema chama hicho kinaamini kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa vitendo vya kukandamiza sauti za kisiasa na kuwatisha wananchi wanaodai haki zao za kiraia.
“Hukumu hii ni mwendelezo wa mbinu za kukandamiza sauti za mabadiliko na kuwatisha wananchi wanaosimamia haki zao za kiraia,” ilisema sehemu ya taarifa ya chama hicho.
Chadema imetangaza kuwa inaendelea na maandalizi ya kuchukua hatua za kisheria, ikiwemo kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. Aidha, chama hicho kimetoa wito kwa wanachama wake na watetezi wa haki za binadamu kuchangia fedha za kulipa faini za wanachama hao wanne, ambazo kwa jumla zinafikia Sh1.2 milioni.
Mnyawami alisema mchango huo ni ishara ya mshikamano kwa wanachama hao huku chama kikiendelea kufuatilia hatua nyingine za kisheria zinazohusiana na shauri hilo.