WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, ametangaza kufuta safari yake iliyokuwa imepangwa kwenda Marekani baada ya kuonyesha kutoridhishwa na kauli za Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya Trump kudai kuwa Meloni alimwomba wapige picha pamoja wakati wa mkutano wa viongozi wa mataifa ya Kundi la Saba (G7), na kwamba alikubali kufanya hivyo kwa sababu alimhurumia.
Kauli hizo zimeibua mjadala mkubwa nchini Italia, huku Meloni akizikanusha vikali na kusema hazina ukweli wowote. Waziri mkuu huyo alisisitiza kuwa hajawahi kumuomba Trump au kiongozi mwingine yeyote kupiga picha kwa namna aliyoeleza rais huyo wa Marekani.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Tajani alisema kauli za Trump zimeivunjia heshima Italia na viongozi wake, na kuongeza kuwa hazikustahili kutolewa kati ya mataifa washirika.
“Kumekuwa na maneno ambayo hayawezi kupuuzwa. Heshima kwa taasisi za Italia na viongozi wake ni jambo la msingi,” alisema Tajani wakati akitangaza kufuta safari yake ya Marekani.