SERIKALI ya Uganda imetangaza Jumanne, 12 Mei 2026 kuwa Sikukuu ya kitaifa ili kuadhimisha kuapishwa kwa Rais mteule Yoweri Kaguta Museveni kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa Urais uliofanyika 15 Januari.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika Uganda Media Centre, Katibu Mkuu wa National Resistance Movement, Richard Todwong, alisema chama hicho kwa kushirikiana na Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi kimejipanga kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa.
Todwong alisisitiza kuwa chini ya mfumo wa vyama vingi, NRM inafanya kazi bega kwa bega na Serikali na inahusika kikamilifu katika maandalizi ya tukio hilo.
Katika matokeo ya uchaguzi, Museveni alipata kura 7,946,772 sawa na asilimia 71.65 ya kura halali. Mpinzani wake Mkuu, Robert Kyagulanyi Ssentamu wa chama cha National Unity Platform, alipata kura 2,741,238 (asilimia 24.72).
Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Nathan Nandala Mafabi wa Forum for Democratic Change aliyepata kura 209,039 (asilimia 1.88), huku wagombea wengine wakipata chini ya asilimia moja.
Kwa mujibu wa Todwong, Chama tawala kilishinda viti 372 kati ya 529 vya ubunge, pamoja na kushika nafasi nyingi katika Serikali za mitaa, ikiwemo nafasi 117 za wenyeviti wa Wilaya.