Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Lameck Jonathan Mlay (30), mkazi wa Maji ya Chai na mfanyakazi wa usafi, kwa tuhuma za kumuua Husna Shabani (33), mkazi wa Majengo jijini Arusha, na kisha kuuficha mwili wake katika chemba ya maji taka. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo 15 Juni 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, amesema tukio hilo lilitokea Juni 14, 2026 katika eneo la Shisha Village lililopo Kata ya Elerai.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa na marehemu walikuwa pamoja katika starehe kabla ya tukio hilo kutokea.
Kwa mujibu wa polisi, mtuhumiwa anadaiwa kumjeruhi marehemu katika sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo chake kabla ya kuutupa mwili huo kwenye chemba ya maji taka.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi ili kukamilisha taratibu za kisheria, huku likitoa wito kwa wananchi kutatua migogoro kwa njia za amani na kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu.