CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimelazimika kurejesha Sh. 918 milioni, zilizotolewa na washirika wa maendeleo kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wa chama hicho Tanzania Bara na Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Jumatatu 15 Juni 2026, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amesema fedha hizo zimerejeshwa kwa kuwa hazikuweza kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa mujibu wa Mnyika, fedha hizo ziliingizwa katika kipindi ambacho chama hicho kilikuwa kwenye kile alichokiita “kifungo” cha zaidi ya siku 300, hali iliyosababisha kushindwa kutekeleza shughuli zilizolengwa za kuwawezesha wanawake wa chama hicho nchini.
Mnyika alieleza kuwa kutokana na kutotekelezwa kwa programu hizo kama ilivyopangwa, Chadema ilichukua hatua ya kuzirejesha fedha hizo kwa wahisani husika kwa kuzingatia masharti ya matumizi ya fedha za miradi.