Waziri wa Sheria na Maendeleo ya Katiba, Mmamoloko Kubayi
SERIKALI ya Afrika Kusini imeeleza wasiwasi wake kuhusu athari za kuongezeka kwa mtazamo kwamba wananchi wake wana chuki dhidi ya wageni, ikisema hali hiyo imeanza kuathiri sekta ya sanaa na burudani nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Afrika Kusini … (endelea).
Waziri wa Sheria na Maendeleo ya Katiba, Mmamoloko Kubayi amesema baadhi ya Wasanii wa Afrika Kusini wameanza kupoteza fursa za kufanya maonyesho katika Mataifa mbalimbali ya Afrika baada ya waandaaji kufuta matamasha yaliyokuwa yamepangwa.
Kubayi amesema baadhi ya wasanii wamemfikia binafsi wakilalamikia kufutwa kwa maonyesho yao katika nchi mbalimbali za Bara hilo, jambo ambalo limeathiri mapato yao pamoja na ukuaji wa sekta ya burudani.
Aidha, Waziri huyo amesisitiza kuwa Afrika Kusini si taifa lenye chuki dhidi ya wageni kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, akionya kuwa taswira hiyo inaweza kuharibu uhusiano wa nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika, pamoja na kuathiri biashara, utalii na uwekezaji.
Hata hivyo, Serikali imewataka wananchi kushughulikia changamoto za uhamiaji kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, ikionya kuwa vitendo au kauli zinazoweza kutafsiriwa kama chuki dhidi ya wageni vinaweza kuleta madhara makubwa kwa uchumi na hadhi ya nchi hiyo ndani ya Bara la Afrika.