JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), ambaye mwili wake ulikutwa umekatwa kichwa na kutupwa katika Mto Msimbazi tarehe 30 Aprili 2026.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Akizungumza na vyombo vya habari leo 6 Mei 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Muliro Jumanne Muliro amesema waliokamatwa ni Steven Rogers Chaka (31), Afisa Maabara mkazi wa Bomang’ombe, Hai mkoani Kilimanjaro, Anna Frank Lema (30), mfanyabiashara mkazi wa Tabata Chang’ombe,Twalibu Khamis (23) na Michael John (26), wote wakazi wa Kigogo Kati jijini Dar es Salaam.

Kamanda Muliro ameongeza kuwa uchunguzi bado unaendelea na kwamba kuna vielelezo mbalimbali vinavyofanyiwa kazi ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
Aidha Muliro ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika na tukio hilo kulingana na ushahidi utakaopatikana.