LICHA ya kukabiliwa na vikwazo vizito kutoka nchini Marekani, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetangazwa rasmi leo, Alhamisi, Oktoba 22, 2026, kuwa mshindi wa Tuzo ya Sakharov kwa mwaka 2026, hatua inayotajwa kuwa ishara thabiti ya uungwaji mkono kutoka Bunge la Ulaya, ingawa inaweza kuzua mtafaruko wa kidiplomasia na utawala wa Rais Donald Trump.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola ameeleza kuwa uamuzi huo umelenga kutambua mchango wa ICC katika kusimamia sheria za kimataifa na haki za binadamu akisema, “Umoja wa Ulaya umejengwa juu ya misingi ya kuheshimu ushirikiano wa kimataifa na taasisi za kimataifa, na tuzo hii inatambua kazi kubwa inayofanywa na mahakama katika kusimamia sheria na haki za kimataifa”.
Uamuzi huu unajiri wiki chache tu baada ya Marekani kutangaza vikwazo vipya dhidi ya ICC kwa madhumuni ya kudhoofisha shughuli zake za kila siku, hatua iliyochochewa na ghadhabu za utawala wa Trump kufuatia mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutokana na tuhuma za uhalifu huko Gaza. Hali hiyo inafuatia pia tuzo ya amani ya Nobel aliyopewa aliyekuwa jaji wa ICC, Navi Pillay, mwezi huu ambayo Trump aliikosoa vikali.
Umoja wa Ulaya umeweka wazi msimamo wake wa kusimama kidete na ICC, ukisema uko tayari kuchukua hatua zote zinazohitajika kuhakikisha mahakama hiyo inaendelea na majukumu yake bila kushinikizwa au kutishwa.
Tuzo hiyo ya kila mwaka, iliyoanzishwa mwaka 1988 kwa heshima ya mwanaharakati wa zamani wa Soviet, Andrei Sakharov, inatambua watu na mashirika yanayopigania haki za binadamu.
Katika kinyanyanyiro cha mwaka huu, ICC imewashinda washindani wengine wawili wa mwisho waliokuwa kwenye orodha ambao ni Tundu Lissu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA ambaye amekuwa kizuizini tangu Aprili 2025 akikabiliwa na mashitaka ya uhaini, na Taraneh na Romina Rahimi ambao ni dada pacha wenye umri wa miaka 21 kutoka Iran, waliohukumiwa kifo na miaka 36 jela kwa kushiriki maandamano ya kupinga serikali nchini humo.