RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, ameruhusu kufanyika rasmi mazungumzo yanayolenga kuachiwa huru kwa mpinzani wake wa muda mrefu Kizza Besigye na Wakili wake Erias Lukwago.Anaandika Joster Mwangulumbi … (Endelea)
Wawili hao wanaokabiliwa na kesi ya uhaini, wakati huu wakiendelea kuzuiwa gerezani wakiwa katika hali mbaya ya kiafya.
Taarifa ya Museveni kuruhusu mazungumzo hayo imethibitishwa na Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba, Norbert Mao.
“Watu wanaohusika, wakiongozwa na Jenerali Sale, wanatekeleza maelekezo ya Rais, ambaye anataka suluhisho la kina—jambo ambalo huenda mahakama ikashindwa kulitoa.
Hivyo, maelekezo ya Rais ni kuzungumza na kila mtu mwenye ushawishi au anayehusika katika maisha ya Erias Lukwago na Dk. Besigye, ili tupate maelewano.
” Ninawahakikishia kuwa mambo yataisha vyema.”
Dk. Besigye na Lukwago, bado wanakabiliwa na mashtaka ya uhaini lakini hivi karibuni Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Lino Anguzo, amesema ataondoa mashtaka iwapo kutakuwa na suluhu ya kisiasa.
“Itakuwa jambo halali kuunga mkono suluhu ya kisiasa kuhusu suala hili. Uhaini ni kosa la kisiasa kwa mujibu wa sheria zetu, hivyo iwapo kutakuwa na suluhu ya kisiasa, ni halali kwa ofisi yangu kuzingatia iwapo suluhu hiyo inahalalisha kusitishwa kwa kesi hiyo,” amesema
Dk. Besigye anasemekana kuwa tayari kwa mazungumzo hayo, lakini sharti la kwanza ni yeye kupewa dhamana.
Haya yameelezwa na Dk. Lulume Bayiga, ambaye aliyemtembelea hivi karibuni.
Mwisho.