CHAMA Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) imesema Serikali ilipuuzia kwa muda mrefu ushauri wa wadau kuhusu umuhimu wa kufanya mageuzi ya Katiba na sheria, hali iliyochangia kuongezeka kwa hasira miongoni mwa wananchi na kusababisha mlipuko wa vurugu.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza hii leo 11 Mei 2026 na waandishi wa habari,Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, alisema chama hicho kilitoa ushauri mapema kabla hali haijaharibika, lakini Serikali haikuwa tayari kusikiliza wala kujadili kiini cha madai ya wananchi.
Mwabukusi alisema kupuuzwa kwa maoni ya wadau kulisababisha wananchi wengi kukata tamaa na kujikuta wakichukua hatua mbalimbali kutokana na hasira waliokuwa nazo.
Aidha, TLS imesema imebaini mambo saba yenye dosari katika taarifa ya Tume ya Jaji Chande, ikiwemo kile ilichodai kuwa ni ukosefu wa uchunguzi wa kina kinyume na hadidu za rejea ilizopewa tume hiyo.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, tume hiyo imetoa maelezo yasiyo na uthibitisho wa kutosha kuhusu matukio ya mauaji, utekaji na kupotea kwa watu, huku ikidaiwa kutegemea zaidi taarifa kutoka vyombo vya dola badala ya kufanya uchunguzi huru na wa kina.
Tamko hilo limetolewa wakati TLS ikizungumzia ripoti ya Tume ya Jaji Chande pamoja na mwenendo wa kesi inayomhusu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.