Wachezaji wa Yanga
KLABU ya Yanga imetozwa faini ya Sh. 30 milioni kwa kosa la wachezaji pamoja na maofisa wa benchi la ufundi kukataa kutumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na badala yake kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja huo, huku Memeja wake, Walter Harson akifungiwa michezo mitatu. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu vyombo vya maamuzi. Mbali na adhabu hiyo, Yanga pia imepewa onyo kutokana na kuchelewa kuwasili uwanjani wakati wa mchezo husika.
Katika hatua nyingine, shabiki wa Yanga aliyefahamika kwa jina la Mohammed Ally Mposo, ambaye amekuwa akiambatana na maofisa wa ufundi wa klabu hiyo, amefungiwa kuingia viwanjani kwa kipindi cha miezi 12.
Mposo amechukuliwa hatua hiyo baada ya kuingia ndani ya eneo la kuchezea wakati wa mapumziko na kumwaga vimiminika, kitendo kilichotafsiriwa kuwa na viashiria vya imani za kishirikina.

Pia kamati hiyo imemfungia michezo mitatu Harson michezo mitatu, pamoja na kumtoza faini ya shilingi milioni moja baada ya kupatikana na hatia ya kumsukuma mchezaji wa Simba, Clatous Chama katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichofanyika tarehe 9 Mei 2026, kufuatia tukio hilo lililotokea wakati wa mchezo huo wa ligi kuu.
Kamati hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo imelenga kulinda nidhamu, heshima na ustaarabu katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.