Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Devotha Minja (Mb), imefanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kujionea utendaji kazi, maendeleo ya huduma pamoja na utekelezaji wa maboresho yanayoendelea katika bandari hiyo.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utoaji huduma bandarini, Mhe. Minja amesema kamati yake imeridhishwa na kiwango cha ufanisi kilichofikiwa na Bandari ya Dar es Salaam, huku akiipongeza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuendelea kuboresha huduma na kuongeza tija.
Amesema maboresho makubwa ya miundombinu na mifumo ya utoaji huduma yameifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa kitovu muhimu cha biashara kwa Tanzania na nchi jirani zinazotegemea bandari hiyo kupitisha mizigo yao. Aidha, alieleza kuwa kasi ya ukuaji wa shehena na ongezeko la meli zinazoingia bandarini ni ishara ya kuimarika kwa ushindani wa bandari hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ( Mb), ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ( PAC) kwa kufanya ziara hiyo na ameihakikishia Kamati kuwa maoni, ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo yatafanyiwa kazi kwa lengo la kuongeza zaidi ufanisi wa huduma bandarini na kuimarisha mchango wa sekta ya bandari katika kukuza uchumi wa Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, IGP Mstaafu Ernest Mangu, aliishukuru PAC kwa ziara hiyo na kueleza kuwa maoni na ushauri wa kamati yataendelea kuboresha utekelezaji wa miradi ya maboresho ya Bandari na kuchangia pia katika kuongeza zaidi ufanisi.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji na uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Bw. Plasduce Mbossa, ameileza Kamati kuwa TPA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na maboresho ya miundombinu ili kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo mingi zaidi kwa wakati na kufafanua kuwa maboresho hayo yamechangia kuongezeka kwa mapato ya ndani ya mamlaka hiyo pamoja na kuimarika kwa ushindani wa bandari katika kuhudumia masoko ya nchi jirani zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la biashara.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuweka rekodi mpya za utendaji ambapo terminal ya makontena ilihudumia makontena 85,243 (TEUs) mwezi Mei 2026, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya bandari hiyo. Mafanikio hayo yanahusishwa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, matumizi ya teknolojia na maboresho ya mifumo ya uendeshaji.
Bandari ya Dar es Salaam ndiyo bandari kuu ya Tanzania inayohudumia takribani asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya nchi na kuhudumia pia nchi zisizo na bandari baharini ikiwemo Zambia, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi na Uganda.