Magari ya mitumba
WATU wanaoagiza magari yaliyotumika (mtumba) nje ya nchi kwa miaka 20, sasa watalazimika kulipa ushuru wa asilimia 50 kutoka asilimia 30 ya awali. Hatua hiyo imelenga kupunguza kiwango cha uchafuzi wa mazingira. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Pendekezo hilo limetolewa bungeni, leo tarehe 11 Juni 2026 na Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akisoma Hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye magari yaliyotumika kwa muda wa miaka minane, 10 na 20.
Serikali pia imependekeza magari yaliyotumika kwa miaka minane na yasiyozidi miaka 10 yatakayoingizwa nchini kulipa ushuru wa asilimia 15 hadi asilimia 20.
“Kwa magari yenye miaka 10 na kuendelea, serikali inapendeza ushuru wa asilimia 40 kutoka asilimia 30, kwa magari yenye miaka miaka 20 tunapendekeza ushuru wa asilimia 50,” amesema Balozi Khamis.
Kwa mujibu wa waziri huyo, mapendekezo hayo yanalenga kuongeza mapato ya Serikali pamoja na kupunguza uingizaji wa magari husika ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababisha uchafuzi wa mazingira kwa asilimia 87 kutokana na uwepo wa taka ngumu ambazo hutumia gharama kubwa katika kuziteketeza.
Wabunge wataanza mjadala wa bajeti hilo na kama pendekezo hilo litapitishwa na wabunge wanaotarajia kuanza kujadili bajeti hiyo, tarehe Juni 14, 2026 litaanza kufanya kazi tarehe 1 Julai, 2026.