RAIS wa Marekani Donald Trump na Rais wa China Xi Jinping wanatarajiwa kujadili masuala ya Iran, Taiwan, akili bandia (AI) na silaha za nyuklia huku wakitathmini uwezekano wa kuongeza muda wa makubaliano muhimu kuhusu madini adimu, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani waliotoa taarifa kabla ya ziara ya Trump nchini China wiki hii. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Viongozi hao wa mataifa mawili yenye uchumi mkubwa duniani watakutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miezi sita, wakijaribu kuimarisha uhusiano ambao umeathiriwa na migogoro ya biashara, vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na tofauti nyingine za kisiasa.
Trump anatarajiwa kuwasili Beijing siku ya Jumatano, kabla ya mazungumzo yatakayofanyika Alhamisi na Ijumaa. Hii itakuwa ziara yake ya kwanza nchini China tangu mwaka 2017.
Marekani na China zinatarajiwa kukubaliana kuunda majukwaa ya kurahisisha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili. Aidha, China inatarajiwa kutangaza ununuzi wa ndege za Boeing pamoja na bidhaa za kilimo na nishati kutoka Marekani, maafisa hao walisema.
Mazungumzo kati ya Trump na Xi yanatarajiwa pia kugusia masuala ambayo kwa muda mrefu yamekuwa chanzo cha mvutano kati ya Marekani na China, ikiwemo Iran, Taiwan na silaha za nyuklia.
China inaendelea kuwa na uhusiano na Iran na ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Iran. Trump amekuwa akiitaka China kutumia ushawishi wake kuishinikiza Tehran kufanya makubaliano na Washington na kumaliza mzozo ulioanza baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran mwishoni mwa Februari.
Utawala wa Trump pia umeishinikiza China kuhusu uhusiano wake na Urusi. Maafisa wa Marekani walisema Trump amezungumza mara kadhaa na Xi kuhusu Iran na Urusi, akieleza wasiwasi kuhusu mapato ambayo China inaipatia nchi hizo pamoja na bidhaa zinazoweza kutumika kijeshi.