WAKULIMA mkoani Morogoro wameiomba serikali kuwasaidia kuwapatia mikopo wakati wa kilimo ili kuepukana na mikopo umiza inayotolewa na watu binafsi yenye riba kubwa wanayoirejesha wakati wa mavuno na kushindwa kunufaika na mfumo wa stakabadhi ghalani. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).
Mkulima mmoja wa Kakao kutoka wilayani Mvomero mkoani Morogoro Samwel Joseph amesema hayo leo kwenye maonesho 88 kanda ya Mashariki kuwa AMCOS nyingi hazijawezeshwa mitaji ya kuwasaidia wakulima kama mikopo kutoka serikalini na kusababisha kujiingiza kwenye mikopo umiza na hivyo kujikuta wakiweka dhamana shamba zima na kukosa kuona faida ya kilimo.
“Utakuta mkulima amekopa fedha za kuandalia shamba na tatizo huja pale akikopa hela nyingi hulazimu shamba lake kuwekwa bondi na Kakao yake kukosa fursa ya soko zuri iliyoandaliwa na serikali kupitia stakabadhi ghalani baada ya mazao yao kutaifishwa na madeni yakiwa shambani kabla ya mauzo” amesema Joseph.
Pia Joseph ameishukuru serikali kwa kuweka mfumo wa stakabadhi ghalani unaowasaidia wakulima kuona tija ya kilimo, kupata fedha na kujenga nyumba za kisasa sambamba na kubadilisha maisha yao na kuishi kama wanaoishi mjini.
Joseph Alfonce ni mkulima wa ufuta na mbaaza katika kijiji cha Sesenga kata ya Mngazi wilayani Morogoro ambaye anasema mfumo wa stakabadhi ghalani umewasaidia wakulima kuwa na bei moja ya mazao na kuepuka kudhurumiwa na walanguzi ambao walikuwa wakipanga wenyewe bei za mazao bila kumjali mkulima.
Meneja wa chama cha ushirika cha wakulima mkoani Morogoro (MOFACU) Andrew Bellah amesema kwa sasa serikali inafanya utaratibu ili kuanzisha Saccos za wakulima kwenye vyama vya ushirika vya msingi(AMCOS) na kuwakopeshwa wakulima kukabiliana na maandalizi ya mashamba kwa ajili ya kilimo.
Amesema wakulima wakipata wepesi kupata mikopo ya maandalizi ha kuuza mazao kupitia stakabadhi ghalani kunamsaidia mkulima kuona manufaa kwa sababu bei ya mazao hupanda kila mwaka na mkulima hulipwa fedha saa 72 baada ya kufikisha mazao hayo kwenye ghala.