BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi rasmi malori 15 yaliyowezeshwa kupitia mkopo wenye riba nafuu kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) na Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Malori hayo yanajumuisha malori 10 kwa KACU na malori Matano kwa TANECU, yakilenga kuboresha ukusanyaji na usafirishaji wa mazao, kuongeza ufanisi wa shughuli za vyama vya ushirika na kuinua kipato cha wakulima.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika katika Maonesho ya Kilimo Nanenane 2026 jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa NBC, Raymond Urassa, alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya benki ya kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo kwa kuwawezesha wakulima kupitia suluhisho bunifu za kifedha.

Naye Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk. Benson Ndiege, aliipongeza NBC kwa mchango wake katika kuimarisha sekta ya ushirika, huku viongozi wa TANECU na KACU wakieleza kuwa malori hayo yataongeza ufanisi wa biashara zao na kuboresha maisha ya wanachama.