KESI ya kupanga njama za kufanya mauaji inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Geita Vijijini, Neema Steven Chozaile, inatarajiwa kutajwa kesho, Jumatano 5 Agosti 2026, katika Mahakama ya Wilaya ya Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Neema anakabiliwa na shtaka la kula njama za kufanya mauaji, kinyume na Kifungu cha 215 cha Kanuni ya Adhabu.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, upande wa Jamhuri unadai kuwa kati ya 1 Septemba 2025 na 29 Juni 2026, katika maeneo mbalimbali ya Wilaya na Mkoa wa Geita, alishirikiana na watu wengine kupanga njama za kuwaua askari wa polisi.
Kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya mwisho, upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa upelelezi ulikuwa umekamilika, hatua iliyosababisha mahakama kuahirisha shauri hilo hadi 5 Agosti 2026 kwa ajili ya hatua zinazofuata za mwenendo wa kesi.
Akizungumza baada ya kesi hiyo kutajwa, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Galubindi alisema mshtakiwa hakufikishwa mahakamani kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hali mbaya ya afya.
Galubindi pia alisema Neema alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa takribani siku 20 kabla ya kufikishwa mahakamani na kusomewa shtaka hilo 20 Julai 2026.
Kesi hiyo inatarajiwa kufuatiliwa kwa karibu kutokana na uzito wa shtaka linalomkabili mshtakiwa na nafasi yake ya uongozi ndani ya Chadema.