Karasira Aimable Uzaramba
MFUNGWA Karasira Aimable Uzaramba amefariki dunia saa chache kabla ya kuachiliwa kwake rasmi kutoka Gerezani, baada ya kumaliza kifungo chake cha miaka mitano nchini Rwanda. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa, Marehemu alimeza kiasi kikubwa cha dawa alizokuwa akitumia kwa ajili ya matatizo ya afya ya akili, katika tukio linalohisiwa kuwa jaribio la kujiua. Karasira alikimbizwa katika Hospitali ya Nyarugenge Hospital, lakini Madaktari walishindwa kumuokoa.
Alikuwa amehukumiwa kwa makosa yakiwemo kuchochea mgawanyiko na kusambaza taarifa za uongo.
Mamlaka zimesema uchunguzi zaidi unaendelea na ripoti rasmi ya kitabibu kuhusu chanzo cha kifo chake inatarajiwa kutolewa.
Alianza kujulikana alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Rwanda kilichopo Butare, kusini mwa nchi, mwanzoni mwa miaka ya 2000. Alikuwa Mwanafunzi katika fani ya sayansi ya kompyuta, akijulikana kwa akili ya juu na uwezo mkubwa wa kitaaluma.
Karasira Aimable Uzaramba alielezewa kama mtu aliyekuwa tofauti na wanafunzi wengine. Alipendelea kujitenga, lakini pia alikuwa na uhusiano mzuri na wanamichezo wa karate chuoni hapo, na hata alikuwa na mkanda mweusi katika mchezo huo.
Ingawa alikuwa Mwanafunzi mwenye mafanikio makubwa kitaaluma, alionekana pia kuwa na changamoto za kisaikolojia au mawazo tofauti na wengine, jambo ambalo baadaye lilijitokeza zaidi katika maisha yake na hata wakati wa kesi yake.
Baada ya kuhitimu kwa alama nzuri, alipata nafasi ya kufundisha katika chuo kikuu cha Rwanda, hatua iliyomfanya aendelee kujulikana katika sekta ya elimu kabla ya maisha yake kuchukua mwelekeo mwingine baadaye.