OFISI ya Veta Kanda ya Dar es Salaam, Chuo cha Chang’ombe, imetangaza fursa za mafunzo bure kwa vijana kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kupata stadi za kazi na kujiajiri. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na ofisi hiyo, jumla ya fani 10 zitahusika katika awamu ya kwanza ya programu hiyo huku kila wilaya ya Mkoa wa Dar es Salaam ikitakiwa kuwa na wanafunzi 1,000 watakaonufaika na mafunzo hayo.
Tangazo hilo limewataka wananchi wenye sifa kujitokeza mapema kuwasiliana kupitia namba zilizotolewa ili kupata taarifa zaidi kuhusu usajili na ratiba za mafunzo hayo. Wilaya zitakazonufaika ni Kigamboni, Ubungo, Ilala, Temeke na Kinondoni.
Tangazo hilo limeeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa bila malipo ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwainua vijana kiuchumi kupitia elimu ya ufundi stadi.
Fani zilizotajwa katika programu hiyo ni pamoja na umeme, useremala, ushonaji na teknolojia ya nguo, ufundi magari, ufungaji na utandazaji bomba, pamoja na utengenezaji wa bodi za magari.
Fani nyingine ni uashi, uungaji na uundaji vyuma, uandaaji wa mapishi ya vyakula pamoja na mauzo ya huduma ya chakula na vinywaji.