MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imeahirisha kutoa uamuzi kuhusu maombi ya zuio yaliyowasilishwa dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Maombi Madogo Na. 14864/2026.Anaripoti Salehe Mohammed, Dar es Salaam … (endelea).
Uamuzi huo ambao ulitarajiwa kutolewa leo 8 Oktoba 2026, sasa utatolewa 22 Oktoba 2026 saa 8:00 mchana.
Awali Said Issa na wenzake watatu (Ahmed Rashid Khamis na Maulid Komu ambaye ni marehemu) walifungua shauri Na. 8323 ya mwaka 2025, mbele ya Jaji Hamidu Mwanga walilalamika kuwa Chadema haifanyi mgawanyo wa rasimali za chama kwa usawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia walidai kuwepo kwa ubaguzi wa kidini kwenye chama hicho.
Chadema hawakuridhishwa na mwenendo wa shauri hilo ikiwa pamoja na kusitishwa kufanya shughuli za kisiasa walikwenda Mahakama ya Rufani kuomba mapitio ya shauri hilo ambapo tarehe 15 Aprili 2026 mahakama hiyo ilifuata zuio hilo la kumuondoa Jaji Hamidu Mwanga kwenye usikilizaji wa shauri hilo.
Tarehe 28 Mei 2026 Jaji David Ngunyale aliyepangiwa kuendelea kusikiliza shauri hilo alilifuta shauri hilo kutokana na dosari za kisheria.
Julai mwaka huu, Said na mwenzake Ahmed walifungua upya shauri hilo lenye madai yale yale.
Akizungumza na MwanaHALISI digital, Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Galubindi, amesema kuahirishwa kwa uamuzi huo kumetokana na Jaji aliyepaswa kutoa uamuzi kuwa na majukumu mengine nje ya kituo chake cha kazi.
Maombi hayo yamewasilishwa na Said Issa Mohamed na Ahmed Rashid Khamis dhidi ya Chadema, huku Mahakama Kuu ikiombwa kuamua kuhusu zuio waliloliwasilisha katika shauri hilo.
Katika shauri hilo, pande hizo zimewasilisha hoja zao mbele ya Mahakama, huku uamuzi wa Mahakama Kuu ukitarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu maombi ya zuio yaliyowasilishwa na waombaji.