MAHAKAMA ya Rufani ya Tanzania iliyoketi jijini Arusha, leo 8 Oktoba 2026, imeamuru Mtendaji wa Mahakama na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), kumrejeshea fedha zote wakili Peter Madeleka, alizolipa kwa ajili ya faini na fidia.Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Katika rufaa hiyo aliyoifungua wakili Madeleka kwenye mahakama hiyo, mwaka 2023 dhidi ya Jamhuri, aliomba nafuu za kisheria ikiwemo kurejeshewa faini.
Msingi wa shauri hilo ni kesi Na 40/2020, ambapo Madeleka alifunguliwa shtaka la uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na alikiri kosa kwa utaratibu wa kulipa faini na fidia.
Hata hivyo wakili Madeleka alikata rufaa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha mwaka 2022, mbele ya Jaji Aisha Bade, kudai fidia aliyolipa kama Plea-Bargain na mahakama itamke kuwa alishtakiwa kinyume cha sheria.
Katika hukumu yake Jaji Bade, aliamuru shauri hilo lirejeshwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa ajili ya kuanza upya.
Madeleka hakuridhishwa na uamuzi huo akienda Mahakama ya Rufaa kuhoji uhalali wake chini ya kifungu cha 21 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code) na kifungu cha 140 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Baada ya kupitia hoja hizo, Mahakama ya Rufani imebainisha kuwa Mahakama Kuu ilikosea kisheria kutoa amri ya kesi hiyo ya uhujumu uchumi kurudiwa upya na hivyo kutangaza kuifuta hukumu yote.
Imeamuru Mtendaji wa Mahakama na DPP kurudisha bila kuchelewa fedha zote ambazo Madeleka alizilipa.
MWISHO.