SHAHIDI wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, John Heche, amemhoji Wakili wa Serikali kuhusu taarifa zilizowahi kutolewa na Humphrey Polepole kufuatia tukio la kupigwa risasi Lissu mwaka 2017.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akihojiwa kwa maswali ya Cross Examination na Wakili wa Serikali, Mwinuka, Heche aliulizwa kama Polepole, ambaye wakati huo alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, aliwahi kutoa taarifa ya kulaani tukio la Lissu kupigwa risasi.
Heche alijibu: “Polepole huyu huyu aliyetekwa au mwingine unayemzungumzia?”
Katika mahojiano hayo, Heche pia aliulizwa kuhusu viongozi mbalimbali waliowahi kutoa kauli kufuatia tukio hilo, akiwemo aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye Heche alisema anakumbuka alitoa taarifa ya kusikitishwa na tukio hilo na kuunda tume ya uchunguzi.
Heche pia alikiri kukumbuka kuwa aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo alifika hospitalini baada ya kikao.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Heche alikanusha kusema kuwa daftari lililokuwa getini kwa nyumba ya Lissu liliondolewa, huku akikiri taarifa kuhusu gari lililodaiwa kumfuatilia Lissu hadi nyumbani kwake aliipata kutoka kwa Lissu mwenyewe.
Kuhusu madai ya mauaji aliyoyataja katika ushahidi wake, Heche aliulizwa ni mauaji mangapi aliyoyashuhudia mwenyewe. Alitaja baadhi ya majina, ikiwemo Chacha Isangora na Chacha Marwa, lakini alipoulizwa kuhusu tukio la Arumeru na kama alishuhudia kifo cha Msafiri Mbwambo, alijibu: “Sikuwepo.”
Mazungumzo hayo ni sehemu ya Cross Examination ya Heche katika kesi inayomkabili Lissu.