KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, ameitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kushiriki katika mchakato wa maridhiano ya kisiasa, akisisitiza kuwa maridhiano hayo hayapaswi kuwa kwa ajili ya vyama vya siasa pekee wala kufungamanishwa na mtu mmoja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kihongosi ameyasema hayo wakati akizungumza katika kipindi cha Clouds 360, ambapo alizungumzia kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche kwamba maridhiano hayawezi kufanyika bila uwepo wa Tundu Lissu.
Kwa mujibu wa Kihongosi, kauli hiyo ni mtazamo binafsi wa Heche na haipaswi kuzuia mchakato wa maridhiano.
“Maridhiano sio kwa ajili ya vyama vya siasa tu. John Heche, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, anaposema maridhiano hadi awepo Tundu Lissu ni utashi wake yeye kwamba yeye anaamini hivyo,” amesema Kihongosi.
Amesema mchakato wa maridhiano unaweza kuendelea huku Lissu akiendelea na kesi yake mahakamani, akisisitiza kuwa suala hilo linapaswa kuachwa kwa vyombo vya sheria.
Kihongosi amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba mahakama itaamua hatma ya kesi hiyo kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza kuwa suala la maridhiano linapaswa kutazamwa kwa mtazamo mpana zaidi na si kulihusisha na mtu mmoja, akieleza kuwa vyama vya siasa ni taasisi zinazoweza kushiriki katika mchakato huo.
“Namshauri waje kwenye maridhiano. Na kama suala Tundu Lissu atoke mahakama itatoa hukumu kadri itakavyoona ana makosa au hana. Chama ni taasisi, sio mtu. Waje kwenye maridhiano,” amesema Kihongosi.
Kauli hiyo inakuja wakati mjadala kuhusu maridhiano ya kisiasa nchini ukiendelea, huku suala la kesi ya Tundu Lissu likiwa miongoni mwa masuala yanayotajwa katika mjadala huo.