BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kuunga mkono jitihada za kukuza nishati safi ya kupikia, uhifadhi wa mazingira, utalii na ubunifu wa vijana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Dhamira hiyo imebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, wakati wa hafla maalum ya mnada wa sanaa za picha iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Kizimkazi, Zanzibar.
Mnada huo, ulioandaliwa na Mwanamke Initiative Foundation (MIF) kwa kushirikiana na Waba Group, ulihusisha picha zinazoonesha uzuri, utamaduni, utalii na urithi wa asili wa Zanzibar. Mapato yake yataelekezwa katika kuunga mkono agenda ya nishati safi ya kupikia na uhifadhi wa mazingira.
Rais Samia aliwataka vijana kutumia sanaa ya picha zaidi katika kutangaza utalii wa Tanzania, akisisitiza kuwa ina fursa kubwa za biashara, ajira na kipato.
Akizungumzia nafasi ya NBC, Sabi alisema benki hiyo iko tayari kuwezesha mnyororo mzima wa nishati safi ya kupikia, huku ikiendelea kuunga mkono ubunifu wa vijana na matumizi ya sanaa katika kuitangaza Tanzania.
Katika hafla hiyo, NBC ilitunukiwa tuzo maalum kutoka kwa Rais Samia kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha tukio hilo na kuunga mkono ajenda ya maendeleo endelevu.
Zaidi ya vijana 200 walishiriki, huku kazi za wapiga picha 15 zikichaguliwa na picha 10 kuuzwa kupitia mnada.