WAANDAMANAJI wawili wameuawa kwa kunyongwa mapema Jumanne nchini Iran baada ya mahakama kutekeleza hukumu zao katika mji wa Isfahan. Utekelezaji huo ulifanyika huku ulinzi ukiimarishwa katika eneo la Alikhani Square kufuatia hofu ya kuzuka kwa maandamano.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Shirika la habari la Mahakama ya Iran, Mizan, limetaja waliouawa kuwa ni Amirhossein Safari na Abolfazl Sepahi, likisema hukumu hizo zilitekelezwa mapema Jumanne kwa saa za nchini humo.
Kesi hiyo ni sehemu ya tukio linalojulikana kama kesi ya Alikhani Square, ambapo vijana 12 walihukumiwa adhabu ya kifo.
Kabla ya kunyongwa kwa wawili hao, wengine wawili walitekelezewa hukumu hiyo 19 Julai.
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na familia ya Safari, ndugu zake waliitwa katika Gereza Kuu la Isfahan kwa kile walichoamini kuwa kingekuwa ziara yao ya mwisho kabla ya hukumu kutekelezwa.
Mamlaka za Iran zinawashutumu washtakiwa hao kwa kuhusika katika mauaji ya maafisa wanne wa usalama pamoja na uchomaji moto na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya Januari, tuhuma ambazo zilisababisha mahakama kutoa adhabu ya kifo.