SERIKALI ya Chad imetangaza nia ya kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ikidai kuwa mahakama hiyo imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na imekuwa na mwelekeo wa kuyalenga mataifa ya Afrika.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Katika taarifa yake, Chad imesema kuwa idadi kubwa ya kesi zinazoshughulikiwa na ICC zinahusu nchi za Afrika, jambo ambalo linaibua maswali kuhusu usawa na haki katika utekelezaji wa majukumu ya mahakama hiyo.
Kwa mujibu wa serikali ya Chad, kesi tisa kati ya 13 zilizoko mbele ya ICC zinahusu mataifa ya Afrika, huku watu sita kati ya saba wanaoshikiliwa na mahakama hiyo wakihusishwa na matukio yaliyotokea barani humo.
Chad imeeleza kuwa hali hiyo inaashiria uwepo wa ubaguzi dhidi ya nchi za Afrika na kwamba ni miongoni mwa sababu zilizoifanya kufikiria kujiondoa katika uanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Hata hivyo, ICC imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa uchunguzi wake hufanyika kwa kuzingatia ushahidi na mamlaka iliyopewa, huku baadhi ya kesi zikianzishwa kwa maombi ya nchi husika au kupitia maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.