Tundu Lissu akiwa mahakamani
MWENYEKITI wa Chama cha Chadema Taifa, Tundu Lissu atawahoji kwa maswali ya dodoso Kamishina Mkuu wa Magereza pamoja na Mkuu wa Gereza la Ukonga kuanzia 1 Julai hadi 3 Julai 2026 katika Shauri la Kikatiba Na. 7300 la Mwaka 2026 mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Shauri hilo lilifunguliwa na Mawakili Paul Kisabo, Kulwa Maduhu na Nashon Nkungu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna Mkuu wa Magereza na Mkuu wa Gereza la Ukonga.
Katika shauri hilo, Mahakama inaombwa kuamua kuhusu masuala mbalimbali ya kikatiba yanayohusu vikwazo vya Jeshi la Magereza dhidi ya Tundu Lissu, mawakili wake, ndugu, viongozi na wanachama wanaomtembelea gerezani.
Kulingana na Wakili Paul Kisabo miongoni mwa masuala yanayolalamikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa viongozi na wanachama kumuona Lissu gerezani, pamoja na vitendo vya askari wa magereza vya kusikiliza mazungumzo kati ya Lissu na mawakili wake wanapofanya mashauriano ya kisheria jambo ambalo linakiuka haki ya faragha na haki ya mawakili kufanya kazi yao kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Katika shauri hilo Tundu Lissu ni miongoni mwa wajibu maombi (Respondents, huku Chama cha Wanasheria Tanganyika kitashiriki kama mdau mwenye maslahi katika shauri (Interested Party) baada ya Mahakama kukubali maombi yake.
Aidha, kutokana na uzoefu wao wa kukumbana na changamoto hizo wanapomtembelea Lissu gerezani kwa ajili ya mashauriano ya kisheria, Lissu anatarajiwa pia kuwahoji mawakili waliofungua shauri hilo ili waweze kuieleza Mahakama kuhusu mazingira halisi wanayokumbana nayo wanapotekeleza wajibu wao wa kitaaluma.
Shauri hilo litasikilizwa kwa njia ya Mtandao mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu Jaji Mruma, Jaji Dkt. Rumisha na Jaji Dk. Longopa. Shauri hili ni miongoni mwa mashauri muhimu ya kikatiba yanayoweza kuweka mwelekeo wa kisheria kuhusu haki ya mawakili kufanya mashauriano ya faragha na wateja wao waliopo mahabusu au gerezani, pamoja na kulinda misingi ya haki ya kupata msaada wa kisheria na usiri wa mawasiliano kati ya wakili na mteja.